3 Machi 2025 - 23:42
Source: Parstoday
Yemen yaionya Israel, Marekani: Tunaitazama Gaza; vidole vyetu viko kwenye kitufe cha bunduki

Harakati ya Ansarullah nchini Yemen imetoa onyo kali dhidi uvamizi wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel unaoungwa mkono na Marekani katika Ukanda wa Gaza, na kusema imejiandaa kikamilifu kuchukua hatua dhidi ya maslahi ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Hazem al-Asad, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah, amesisitiza kwamba harakati hiyo "imejiandaa kushiriki katika vita vikubwa vitakavyolenga maslahi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi" ikiwa uchokozi utaendelea.

Ameitahadharisha Marekani kuhusu uungaji mkono na himaya yake kwa utawala ghasibu wa Israel katika mashambulio yake dhidi ya watu wa Gaza au uchokozi wowote dhidi ya Yemen.

Akisisitiza msimamo huo, Nasr al-Din Amir, afisa mwingine wa ngazi ya juu wa Ansarullah, amesema: "Macho yanatazama Gaza, na vidole vyetu viko kwenye kitufe cha kufyatua risasi."

Amesisitiza kuwa makombora, ndege zisizo na rubani na vitengo vyote vya Jeshi la Yemen viko tayari kabisa, akisema, "Tumethibitisha uwezo wetu katika majaribio ya hapo awali."

Amir alikuwa akiashiria mashambulizi ya vikosi vya Jeshi la Yemen dhidi ya maeneo nyeti ya Israel na Marekani katika eneo la Asia Magharibi pamoja na meli za Israel au meli zinazopeleka bidhaa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, kufuatia kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza Oktoba 2023.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha